Masharti haya yanaeleza matumizi ya Rafiki Pharmacy System. Kwa kufungua akaunti au kulipa kifurushi, unakubali masharti haya kwa niaba yako au ya biashara uliyoidhinishwa kuwakilisha.
1. Huduma ya Rafiki
Rafiki hutoa zana za mauzo, stoo, dawa, wauzaji, fedha, wafanyakazi na ripoti. Vipengele vinaweza kuboreshwa kwa muda. Rafiki si mfamasia, daktari, mhasibu wala wakili; wataalamu wanaotakiwa bado ni wajibu wa mteja. Risiti za TRA zinatolewa tu pale famasia imeunganishwa na TRA kupitia cheti chake cha VFD.
2. Kifurushi na malipo
Kifurushi cha Rafiki Pharmacy kinajumuisha tawi moja, hadi wafanyakazi 10 na vifaa 5. Bei ni TZS 35,000 kwa siku 30, TZS 140,000 kwa siku 180, au TZS 1,500,000 mara moja kwa umiliki wa kudumu, isipokuwa makubaliano mengine ya maandishi. Ufikiaji huanza baada ya malipo kuthibitishwa. Una siku 7 za kughairi malipo na kurudishiwa pesa kama hujaanza kutumia mfumo (Sheria ya Miamala ya Kielektroniki 2015, kifungu cha 30). Baada ya hapo ada za muda ulioanza hazirejeshwi isipokuwa sheria itake vingine.
3. Lipa mara moja, mfumo ni wako
Baada ya malipo ya TZS 1,500,000 ya umiliki wa kudumu, au malipo 12 ya siku 30 mfululizo bila kukatika zaidi ya siku 7 za neema, famasia inapata leseni ya kudumu ya kutumia Rafiki: leseni isiyo ya kipekee, isiyohamishika, kwa famasia moja, bila malipo mengine ya kifurushi. Rafiki inaendelea kuhost mfumo bila ada ndani ya mipaka ya kifurushi iliyokuwepo siku ya leseni. Haki miliki ya programu inabaki kwa Rafiki; famasia haiwezi kuiuza wala kuisambaza kwa wengine. Huduma za ziada zinazogharimu Rafiki pesa kwa kila famasia, kama risiti za TRA kupitia mtoa VFD, SMS na matawi ya ziada, zinalipwa tofauti kadri zinavyotumika. Marekebisho ya usalama yanajumuishwa siku zote.
4. Wajibu wa mteja
Mteja atatoa taarifa sahihi, atalinda password na PIN, atasajili vifaa vinavyofaa, atampa kila mtu ruhusa sahihi, atakuwa na leseni na wataalamu wanaohitajika, na atakagua stoo, bei, mauzo na ripoti. Mfumo hautumiki kwa udanganyifu, kuvunja sheria au kujaribu kufikia famasia nyingine.
5. Kuisha na kusimamishwa
Kifurushi cha muda kikiisha kuna siku 7 za neema kufanya malipo upya. Baada yake ufikiaji unaweza kusimamishwa hadi malipo yathibitishwe. Leseni ya kudumu haisimamishwi kwa kutolipa. Kusimamishwa hakufuti rekodi. Tunaweza kusimamisha akaunti inayohatarisha usalama au kuvunja masharti haya, na tutatoa njia ya kuwasiliana inapowezekana.
6. Data yako na mwendelezo
Data yote ya famasia, dawa, stoo, mauzo, wateja na ripoti, ni mali ya famasia. Mmiliki anaweza kupakua data yote (CSV na SQL) kutoka kwenye akaunti yake wakati wowote, hata mfumo ukiwa umesimamishwa; Rafiki inahakikisha nakala inapatikana ndani ya siku 7 za kuomba. Famasia yenye leseni ya kudumu inaweza pia kupakua bundle ya kujihost yenye programu, muundo wa database na data yake. Kama Rafiki itasitisha huduma hii, itatoa notisi ya siku 90, bundle ya kujihost na msaada wa kuhamisha. Rafiki inashughulikia data kama mchakataji chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2022, kwa maelekezo ya famasia, na haitoi data ya famasia kwa wengine. Famasia inabaki mdhibiti wa data na inawajibika kujisajili PDPC.
7. Upatikanaji na mipaka
Tutafanya juhudi za kitaalamu kuweka huduma salama na ipatikane, lakini mtandao, vifaa, watoa malipo na matukio yaliyo nje ya uwezo wetu yanaweza kusababisha usumbufu. Pale sheria inaporuhusu, dhima ya Rafiki haitazidi ada iliyolipwa kwa kipindi cha sasa, au kwa leseni ya kudumu, ada ya mwaka wa mwisho uliolipwa.
support@rafiki.co.tz